SIMBA SASA YAJIPANGA KIMYAKIMYA KUEPUKA YALIYOWAKUTA KWA MKUDE


Uongozi wa klabu ya Simba umeamua kujipanga ili kuepuka suala la kuendelea kubembeleza wachezaji kila unapowadia wakati wa kusaini mkataba mpya.

Uongozi wa Simba umechoshwa na wachezaji wake kuendelea kuifanyia ngebe kila linapofikia suala la kusainishana mkataba.

Mmoja wa viongozi wa Simba walio kwenye kamati ya utendaji amezungumza na SALEHJEMBE na kusema watahakikisha kila namba ina zaidi ya mchezaji mmoja.

“Tungependa kuwa na wachezaji waelewa, lakini tunapenda kuwa na njia sahihi za kupita. Si ikifika wakati wa mazungumzo ya kuongeza mkataba, basi mnaanza kutafutana na mchezaji, mara wazime simu, mara hawataki kuzungumza na nyie.

“Wakati mwingine unajiuliza, kwa nini mtu asikae na nyie na kusema sitasaini kuliko akimbie. Au akatae kuzungumza na nyie,” alisema kiongozi huyo akionyesha kujiamini.

“Au kama anaona anachopewa hakitoshi, kwa nini pia asiseme. Hivyo ni bora kuepukana na utaratibu wa kumtegemea mchezaji mmoja na badala yake kutegemea timu. Bora kutegemea yoyote kati ya watu watatu hata kama wanazidiana vipi. Maana wachezaji wengi wakitegemewa, wanajisahau. Sasa tumejifunza sana, awali tulibweteka kwa kuwa tulijua wanaipenda sana timu pia baada ya mkataba wangekaa na kujadiliana nasi bila ya mizunguko.

“Mfano mchezaji mmoja akiondoka, basi unaweza kuendelea na mwingine. Au mmoja akianza kuringa bila sababu za msingi, mnasajili mwingine. Simba ni kubwa na watu wanapaswa kuipa heshima yake.”

Hivi karibuni, Simba ililazimika kufanya usajili wa kiungo James Kotei kutoka nchini Ghana baada nahodha wake, Jonas Mkude kuwazimia simu viongozi.

Juhudi za kumpata zilishindikana hadi mwenye alipoungana na timu kwa ajili ya kuanza maandalizi ya mzunguko wa pili.

Hilo lilionyesha wazi kuwakera viongozi wa Simba ambao wamemsajili Kotei kwa miezi sita.

SIMBA SASA YAJIPANGA KIMYAKIMYA KUEPUKA YALIYOWAKUTA KWA MKUDE SIMBA SASA YAJIPANGA KIMYAKIMYA KUEPUKA YALIYOWAKUTA KWA MKUDE Reviewed by Unknown on 1:58 PM Rating: 5

No comments:

Theme images by Colonel. Powered by Blogger.