Adios Twite, vazi la ukimataifa limekutoa Jangwani
Na Abdul Mkeyenge
NIMEREJEA zangu Dar es Salaam jana jioni na leo asubuhi
nimeamka mapema nikiwa na kazi moja tu. Nina kazi ya kuitafuta shajara
yangu inayomuhusu Mbuyu Twite, kile kipande cha baba cha Yanga chenye
damu ya Kongo na kiliwahi kuvaa jezi za timu ya taifa Rwanda ‘ Amavubi
‘.
Katika pitia pitia shajara mbele ya meza iliyofutwa vyema
pembeni kukiwa na kikombe cha kahawa na vitabu vya Ben Mtobwa naenda
kurasa niliyoandika neno historia na moja kwa moja nakutana na kitu
kinachoitwa usajili wa Twite. Haraka sana nafungua kurasa hiyo na
nakukumbuka Agosti 30 siku ya Alhamisi mwaka 2012, Twite ndio alitua
uwanja wa Ndege wa Mw. Nyerere na kulakiwa na manazi wa Yanga
waliomvesha jezi namba 4, huku jezi hiyo ikiandikwa jina la aliyekuwa
Mwenyekiti wa Simba Ismail Aden Rage, wakati huo.
Nderemo, vifijo, raha na mikogo vilitamalaki uwanjani hapo
na Twite mwenyewe hakuwa na mengi ya kusema zaidi ya kushukuru kila
mmoja aliyeenda kumpokea na kusema ” Kujia kwa watu wingi kwa ajili ya
kunipokea inaonyesha Yanga ni timu kubwa na hii itanifanga kufanga kazi
nzuri kwa bidii. Naomba ushirikiano huu udumu na kung’a kitu tutafanga
kama timu” alisema Twite ambaye alizungumza kwa kiswahili kigumu kidogo.
Maneno haya yalitoa milipuko ya kelele kwa watu wa Yanga
waliokuwa uwanjani pale wakimsikiliza na yalikuwa shubili upande wa
Simba ambao nao walitajwa kumsajili na walishaitengeneza hadi jezi yake
na kuiuza katika tamasha lao la kila mwaka la Simba Day.
Mashabiki wa Simba wakati huo waliamini kumpata Twite
kutaenda kuwapoza machungu ya kumpoteza mlinzi wao kinga’ng’anizi Kelvin
Yondani ambaye alitimkia Yanga.
Usajili wa Twite Yanga uliwatoa povu watu wa Simba. Mara
nyingi kwenye majukwaa yao Twite alikuwa na maisha magumu. Alizomewa na
kila mmoja na mwishowe akawa anaitwa jina la Mwizi. Jina hili lilidumu
na lilikuja kupungua makali Simba ilipomsajili Juuko Mursheed.
Lakini Simba ilipokuwa na mabeki Komambil Keita ( Mali ),
Lino Musombo ( Congo ), Obadia Mungusa ( Tanzania ) Pascal Ochieng (
Kenya), jina la Mwizi halikukauka vinywani mwa mashabiki wa Simba.
Kufumba na kufumbua yule Twite aliyewadengulia Simba na
kuwapa pepo ndogo Yanga ametemwa Yanga na nafasi yake imechukuliwa na
Justice Zullu waliomuona wanamuita Mkata Umeme.
Maisha ya mpira ndio yako hivi. Kuna wakati yanakuwa hivi
na wakati yanakuwa vile. Kalamu yangu haiamini kilichofanya Twite
anyimwe mkataba mpya ni uwezo wake kushuka au kama wasemavyo wengine
umri mkubwa.
Twite bado ana nishati ya kucheza Ligi yetu kwa misimu
mitatu mbele bila matatizo. Tukiri leo. Ligi yetu ni dhaifu na haiwezi
kumshinda mchezaji anayejitambua kama Twite kucheza vyema na kuisaidia
timu kupata mataji. Kama tunakiri Twite hana nishati ya kucheza ligi
yetu hapo hapo tujiuluze ni mchezaji yupi wa Tanzania anayemkaribia kwa
ufiti?
Wachezaji wa aina yake hawako tena siku hizi. Tuna
wachezaji wepesi ambao hawako fiti. Kando ya Twite unaweza kumpata
kiraka wa Azam yule mwenye moyo wa Simba na miguu ya chuma Himid Mao.
Angalau Himid anaweza kupishana na Twite linapokuja suala la ufiti.
Kilichomuondoa Twite ni idadi 7 ya wachezaji wa kigeni.
Hapa kulikuwa hakuna namna ilikuwa lazima aache nafasi yake iende kwa
Zullu nae aondoke. Unadhani Twite angezaliwa kwetu Rufiji angeondoka
Yanga na kumuacha Said Makapu? Kuzaliwa Kinshasa ndio kumemnyima
mkataba.
Timu nyingi zinatamani huduma yake. Amini hili. Hata hao
waliokuwa wakimzomea hawakumzomea kwa kuwa Twite alikuwa hajui mpira,
walimzomea ni kutokana na kuwahi kuwauzi.
Licha ya hivyo malipo ya Dola Elfu mbili kwa TFF nayo ni
sababu nyingine inayofanya baadhi ya timu kuishia kumtamani kutokana na
kutokuwa na uwezo wa kumlipia fedha hizo.
Twite anakupa vitu vingi mchezoni. Anakupa faida ya
kujilinda na kushambulia, huku akiwa na faida ya ziada ya kucheza namba
nyingi kwa wakati mmoja. Unadhani angekuwa Mndengereko kama mimi Yanga
ingemuacha? Isingemyacha.
Faida yake nyingine ni mipira ya kurusha. Yanga imevuna
mabao mengi kwa mtindo wake wa kurudi nyuma na kurusha mipira ambayo
mingi inakuwa madhara langoni mwa wapinzani. Yanga walikuwa na style
nyingi za kupata mabao. Kuondoka kwa Twite wamepunguza style moja.
Mipira ya kurusha ina faida. Ukitaka kuliamini hili
tembelea uwanja vya Britania Stadium pale England kisha taja jina la
Delap. Delap aliishi katika sayari yake lilipokuja suala la kurusha
mipira na kuipa timu ushindi.
Lakini nyumbani Twite alibezwa na baadhi ya mashabiki na
akaitwa jina la mcheza rede kutokana na style hiyo. Ninachoamini
kilichomtoa Twite ni ‘uwepesi’ wake katika wachezaji wa kigeni wa Yanga
walioko sasa.
Unaanzaje kufikiria kulikata jina la Niyonzima ambaye
anatajwa kama Nyerere wa Jangwani? Inasemekana Niyonzima ndio
aliyesababisha mmoja ya kiongozi kujiuzulu nafasi yake, mchezaji huyu
unaanzaje kumgusa wewe Lwandamina au Hans?
Tuwakate Donald Dombo Ngoma na Thaban Skalah Kamusoko na
kumpisha Zullu? Hapana! Tuwakate Tambwe Amissi Jocelyn na Vicent Bossou
kumpisha Zullu? Hapa hakukuwa na namna nyingine ilikuwa ni lazima Twite
awe mbuzi wa kafara ili maisha mengine yaendelee Jangwani.
Nilitamani kuendelea kumtazama Twite akiwa na Yanga, lakini
kwa hali iliyoko sioni wapi naweza kumuona kwa wakati huu zaidi ya
kwenda kesho uwanja wa Uhuru kumtazama katika mchezo maalum dhidi ya JKU
ambao utakuwa wa kumuaga.
Nitaenda kuutazama mchezo huu kwa sababu mbili. Mosi
kuagana na Twite ambaye namtakia maisha mema huko aendako na pili
kumtazama huyo Zullu ‘Mkata Umeme’.
Rafiki yangu Peter Kadutu siku za karibuni amekuwa
akijifunza Kihispanyola na moja ya maneno niliyowahi kuyapata kwake ni
neno la Adios likimaanisha kwaheri. Si vibaya nami nikimuaga Twite kwa
kumwambia Adios Twite, vazi la ukimataifa limekutoa Jangwani.
Adios Twite, vazi la ukimataifa limekutoa Jangwani
Reviewed by Unknown
on
6:18 AM
Rating:
No comments: