MECHI ZA FUNGA MWAKA LIGI KUU TANZANIA BARA HIZI HAPA

MTIBWA SUGAR

Mechi 14 za Ligi Kuu ya Vodacom zinatarajiwa kufanyika wakati huu wa msimu wa kufunga mwaka 2016 na mbili za zitafungua mwaka 2017 ambako Kituo cha Televisheni cha Azam - Wadhamini wenza wa ligi hiyo, wamethibitishia Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupata burudani kwa michezo yote kulingana na ratiba.
Katika Ligi hiyo ambayo pia inabarikiwa na Benki ya Diamond Trust (DTB), michezo 15 ya kipindi cha sikukuu za kufunga na kufungua mwaka inatarajiwa kuanza saa 10.00 jioni isipokuwa ule wa Mbao FC na Mwadui uliopangwa kuanza saa 8.00 mchana kama itakavyojieleza hapo chini kwenye mtiririko wa ratiba.
Burudani kwa Wote katika michezo hiyo kutoka Azam Tv, zinaanzia mchezo wa kesho Ijumaa wa Desemba 23, mwaka huu ulipewa jina la Na. 129 utakaozikutanisha timu za African Lyon na Young Africans kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Kamishna wa mchezo anatarajiwa kuwa Idelfonce Magali kutoka Morogoro.
Katika mchezo huo unaotarajiwa kuchezeshwa na Mwamuzi, Ludovic Charles kutoka mkoani Tabora akisaidiwa na John Kanyenye wa Mbeya (Mshika Kibendera Na. 1) na Alnord Bugado wa Singida (Mshika Kibendera Na. 2), Mwamuzi wa Akiba – Mezani anatarajiwa kuwa Israel Nkongo kutoka Dar es Salaam.
NDANDA FC
Jumamosi Desemba 24, 2016 kutakuwa na mechi sita ukianzia ule wa Mbeya City na Toto Africans zitacheza kwenye Uwanja wa Sokoine jijiji Mbeya katika mchezo Na. 130 utakaosimamiwa na Kamishna George Komba wa Dodoma wakati Mwamzi wa kati atakuwa Shakaile ole Shangalai wa Pwani huku wasaidizi wake wakiwa ni Khalfan Sika pia wa Pwani na Vecent Milabu wa Morogoro. Mwamuzi wa akiba atakuwa Cherles Mwamlima.
Mchezo Na. 131 utazikutanisha timu za Kagera Sugar na  Stand United katika Uwanja wa  Kaitaba, uliko Kagera ambako utasimamiwa na Kamishna Nassoroi Hamduni wa Kigoma huku Mwamuzi akiwa ni Jacob Adongo wa Mara akisaidiwa na Joseph Masija na Robert Luhemeja kutoka Mwanza na Mezani atakuwa  Jonesia Rukyaa wa Kagera.
Ndanda itaendelea kubaki nyumbani kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara na baada ya kucheza na Simba juma lililopita na kupoteza mchezo huo, safari hii inaikaribisha Mtibwa Sugar ya Morogoro katika mchezo Na. 132 utakaosimamiwa na Kamishna Jimmy Lengwe wa Morogoro wakati Mwamuzi atakuwa Andrew Shamba wa Pwani akisaidiwa na Haji Mwalukuta wa Tanga na Jeremiah Simon wa Dar es Salaam. Mezani atakuwa Abubakar Mtulo.
Siku hiyo pia kutakuwa na mchezo kati ya Simba na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Mchezo huo Na. 133 utafanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam ambako utasimamiwa na Tito Haule wa Morogoro na kuchezeshwa na Mwamuzi Hans Mabena wa Tanga. Mabena atasaidiwa na Omari Kambangwa wa Dar es Salaam na Khalfan Sika wa Pwani wakati Mbaraka Rashid wa Dar es Salaam atakuwa Mwamuzi wa Akiba – mezani.
Baada ya kulala Mbeya mbele ya Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine, Majimaji ya Songea itakuwa mwenyeji wa Azam FC ya Dar es Salaam ambayo juma lililopita iliambulia sare tasa kutoka kwa African Lyon. Majimaji na Azam zinakutana kwenye mchezo Na. 134 utakaofanyika Uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Katika mchezo huo ambao Mwamuzi atakuwa Ngole Mwangole wa Mbeya ambaye ni mwamuzi bora wa Ligi Kuu ya Vodacom msimu uliopita, atasaidiwa na Mirambo Tshikungu na Mashaka Mwandembwa – pia wote wa Mbeya huku kamishna akiwa ni David Lugenge wa Iringa.
Mwadui ambayo ilianza vibaya duru la pili kwa kupoteza mchezo uliopita, Jumamosi Desemba 24, mwaka huu itakuwa mwenyeji wa Mbao FC ya Mwanza kwenye Uwanja wa Mwadui Complex mkoani Shinyanga. Mchezo huo Na. 135, utasimamiwa na Kamishna Staricko Nyikwa wa Singida katika mchezo utakaoanza saa 8.00 mchana ili kutoa fursa kwa mdhamini Azam kuonesha mchezo huo moja kwa moja ikiwa na maana ya mubashara.
Waamuzi wataongozwa na  Emmanuel Mwandembwa atakayesimama katikati kupuliza filimbi huku akisaidiwa na Abdallah Uhako na Agnes Pantaleo wote wa Arusha na mezani anatarajiwa kuwa Ezekiel Mboi wa Shinyanga.
Krismas, yaani Desemba 25, 2016 hakutakuwa na mchezo ila siku inayofuata Desemba 26, mwaka huu Ruvu Shooting itakuwa mwenyeji wa Tanzania Prisons ya Mbeya kwenye Uwanja wa Mabatini, ulioko Mlandizi mkoani Pwani katika mchezo Na 136.
Manyama Bwire wa Dar es Salaam atakuwa Kamishna wa mchezo huo wakati Mwamuzi ni Forentina Zabron wa Dodoma akisaidiwa na Hassan Zani wa Arusha na Silvester Mwanga wa Kilimanjaro. Mwamuzi wa akiba - Mezani atakuwa Andrew Shamba wa Pwani.
Desemba 28, mwaka huu kutakuwa na mechi mbili ambako Young Africans ya Dar es Salaam itakuwa mwenyeji wa Ndanda ya Mtwara kwenye Uwanja wa Uhuru jijini katika mchezo Na. 137 ambako Juma Chiponda wa Tanga atakuwa kamishna wa mchezo huo.
Mwamuzi wa kati katika mchezo huo atakuwa Eric Onoca wa Arusha akisaidiwa na Michael Mkongwa wa Njombe na Janeth Balama wa Iringa. Mwamuzi wa akiba atakayekaa mezani atakuwa Mwanahamisi Matiku wa Dar es Salaam.
Kadhalika siku hiyo, Majimaji ya Songea itakuwa mgeni wa Mtibwa Sugar ya Morogoro kwenye Uwanja wa Manungu ulioko Mvomero katika mchezo Na. 138 utakaosimamiwa na Kamishna Pius Mashera wa Dodoma, utachezeshwa na Mathew Akrama kutoka Mwanza akisaidiwa na Abdallah Rashid wa Pwani na Gasper Ketto wa Arusha. Mwamuzi wa akiba atakuwa Selemani Kinugani.
Kadhalika Desemba 29, mwaka huu kutakuwa na mechi mbili. Ruvu Shooting ya Pwani inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Simba ya Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam katika mchezo ambao mwamuzi atakuwa Alex Mahagi wa Mwanza.
Katika mchezo huo Na. 139, Mahagi atasaidiwa na Ferdinand Chacha pia wa Mwanza na Rashid Zongo wa Iringa huku mwamuzi wa akiba akiwa ni Hellen Mduma wa Dar es Salaam. Kamishna wa mchezo atakuwa Peter Temu wa Arusha.
Azam ya Dar es Salaam itatulia nyumbani Uwanja wa Azam huko Chamazi ikicheza na Tanzania Prisons ya Mbeya katika mchezo Na. 140 utakaosimamiwa na Elizabeth Kalinga wa Mbeya huku Mwamuzi akiwa ni Jimmy Fanuel wa Shinyanga huku wasaidizi wake wakiwa ni Makame Mdog pia wa Shinyanga na Abdallah Mkomwa wa Pwani huku Kassim Mpinga akiwa ni mwamuzi wa akiba.
Saa kadhaa kabla ya kuingia mwaka 2017, yaani Desemba 31, mwaka huu kutakuwa na michezo miwili ambako Mwadui ya Shinyanga itacheza na Kagera Sugar ya Kagera kwenye Uwanja wa Mwadui mkoani Shinyanga katika mchezo Na.  141.
Kamishna anatarajiwa kuwa Nassib Mabrouk wa Mwanza na Mwamuzi ni Isihaka Mwalile na wasaidizi wake ni Hellen Mduma na Omary Kambangwa – wote kutoka Dar es Salaam. Julius Kasitu wa Shinyanga anatarajiwa kuwa Mwamuzi wa Akiba.
Kadhalika siku ya funga mwaka, Mbeya City inatarajiwa kucheza na Mbao FC kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya katika Mchezo Na. 143 ambao msimamizi wa mchezo atakuwa Joseph Mapunda wa Ruvuma.
Mwamuzi katika mechi hiyo anatarajiwa kuwa Hussein Athuman wa Katavi wakati wasaidizi wake watakuwa ni Lulu Mushi wa Dar es Salaam na Nicholaus Makaranga wa Morogoro. Mwamuzi wa Akiba Mezani atakuwa Mashaka Mwandembwa wa Mbeya.
Januari mosi kutakuwa na michezo miwili tu ya kukaribisha Mwaka Mpya ambako Toto African ya Mwanza itacheza na Stand United ya Shinyanga kwenye Uwanja wa CCM Kirumba katika mchezo Na. 144 utakaosimamiwa na Jovin Bagenda wa Kagera. Mwamuzi atakuwa Israel Nkongo sambamba na wasaidizi wake Soud Lila na Frank Komba, wote wa Dar es Salaam. Mwamuzi wa akiba mezani atakuwa Mathew Akrama wa Mwanza.
Pia African Lyon ya Dar es Salaam itakuwa mwenyeji wa JKT Ruvu katika mchezo Na. 142 utakaofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Kamishna atakuwa Hamisi Kitila wa Singida wakati Mwamuzi anatarajiwa kuwa Selemani Kinugani wa Morogoro wakati wasaidizi wake ni Omary Juma wa Dodoma na Agnes Pantaleo wa Arusha wakati mezani atakuwa Shafii Mohammed wa Dar es Salaam.
Mara baada ya michezo hiyo, Ligi Kuu ya Vodacom itasimama kwa wiki mbili kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi inayotarajiwa kuanza Januari mosi, mwaka huu.
MECHI ZA FUNGA MWAKA LIGI KUU TANZANIA BARA HIZI HAPA MECHI ZA FUNGA MWAKA LIGI KUU TANZANIA BARA HIZI HAPA Reviewed by Unknown on 2:12 PM Rating: 5

No comments:

Theme images by Colonel. Powered by Blogger.