KWA SUALA LA JERRY MURO, KATIBU MKUU TFF ANGEACHIA NGAZI TU
Na Saleh Ally
KARIBU
wiki yote iliyopita, gumzo la Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa
klabu ya Yanga, Jerry Muro ambaye alitakiwa kufikishwa kwenye kamati ya
maadili iliyokuwa inakutana juzi Jumamosi.
Juni
29, mwaka huu, TFF ilimwandikia barua Muro yenye kumbukumbu namba
TFF/ADm/LM.47/2016 ikimtaka kuhudhuria katika kamati ambayo ingekutana
Jumamosi kujibu mashitaka mawili ya kupingana na maamuzi ya TFF, pia
kulishambulia shirikisho hilo kwenye vyombo vya habari.
Kamati
ya Maadili ilishindwa kusikiliza shauri la Muro baada ya kuonekana
barua aliyoandikiwa haikuwa ikieleza atakwenda kusikilizwa na kamati
ipi, licha ya kwamba ya maadili ndiyo ilikuwa inakutana siku hiyo.
Muro
ametumia nafasi hiyo kuchomoka kwenye ‘msala’ huo ambao kiundani
unaonekana unatokana na ile ishu ya Yanga kuamua kuwaingiza mashabiki
wote bure katika mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya TP Mazembe,
Jumanne iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kipindi
hicho, ndicho Muro alionekana kucharuka sana. Aliendelea kueleza
msimamo wa Yanga na ambacho hawakukubaliana nacho. Kama unakumbuka wiki
chache zilizopita hali ilikuwa hivyo wakati wa ubishani wa uchaguzi wa
klabu hiyo usimamiwe na TFF au Yanga na mwisho klabu ikashinda. Mwisho
wa uchaguzi, Rais wa TFF, Jamal Malinzi akaipongeza kwa kufanya uchaguzi
na kupata viongozi wake!
Safari
hii, Muro amechomoka baada ya mwenyekiti wa kamati ya maadili, Wilson
Ogunde kuitaka TFF kumuandikia barua nyingine Muro kwa ajili ya kumuita
kwenye kamati hiyo.
Ogunde
amesema hivyo, kwa kuwa anakiri kweli barua aliyoandikiwa Muro ilikuwa
na mapungufu na haukusema anakwenda kuhojiwa na kamati ipi na hapo ndipo
ninapoanzia.
Kwamba
Katibu Mkuu wa TFF, anashindwa hata kuanzika barua sahihi ya wito wa
mtu ambaye anakwenda kwa ajili ya kuhojiwa na kamati fulani. Kwangu
naona hiki ni kichekesho cha karne.
Mwesigwa
Selestine ndiye mtendaji mkuu wa TFF, baba wa michezo Tanzania! Halafu
hata barua moja ya kutoa maelekezo kama hayo, nayo anashindwa kuiandika
kwa usahihi.
Ninaamini
atakuwa amendika mwenyewe, ninaamini MWesigwa hawezi kuwa amekopi barua
ya zamani na badala yake hiyo iliandikwa upya kabisa kwa ajili ya Muro,
lakini imegeuka kichekesho.
Mtuhumiwa
kashinda hata kabla ya kuhojiwa kutokana na mapungufu ya msingi ndani
ya barua ya taarifa ambayo iliandikwa na katibu mkuu wa shirikisho. Hapa
kinachofuata kwa mtu muungwana ilikuwa ni kujiuzulu kwa picha
inayoonyesha udhaifu wa juu kabisa.
Binafsi
nimejiuliza maswali kibao, kama kweli mtendaji mkuu wa shirikisho
anashindwa hilo dogo kabisa ambalo hata katibu muktasi angelifanya bila
kupindisha, vipi kuhusiana na umakini wa mambo mazito yanayopita ndani
ya shirikisho.
Muro
ambaye ni msemaji wa Yanga, anaonekana kuwa makini na mwelewa wa mambo
hata kuliko katibu mkuu wa shirikisho! Ameweza kutumia udhaifu wa katibu
mkuu kuzuia zoezi la kumhoji, sasa Mwesigwa anatakiwa na kamati kumuita
tena, kama akifanya itakuwa aibu nyingine kubwa sana.
Siamini
kama TFF inapaswa kumziba kila mtu mdomo, kila anayetaka kujitetea.
Ndiyo maana wakati alipofungiwa kimagumashi Dk Damas Ndumbaro
niliwaeleza wadau walivyokuwa wakimya wakati watu ‘wananyongwa’ kwa
hujuma.
Leo
TFF imeshindwa kufikia lengo lake kwa kuwa inafanya mambo kwa jazba.
Wote mnakumbuka ilivyoanza kulazimisha kumtuliza Haji Manara wa Simba.
Kitu kibaya zaidi, watu wa soka tatizo la msingi ambalo linaonekana si
sawa hasa uonevu wa upande mmoja unapotokea, huona ni la upande huo na
wanasahau linaweza kurudi kwingine, kama ambavyo safari hii lilivyokuwa
linakwenda kuwaangukia Yanga kupitia Muro.
Vizuri
kabisa, Mwesigwa naye angepumzika kwa kuonyesha wazi hawezi kuwa makini
kwenye majukumu makubwa ya juu kama ameshindwa kuandika barua tu. Bila
viongozi makini hakuna maendeleo katika soka, makosa yanayoonekana
madogo, ndiyo makubwa yanayotukwamisha. Tusidanganyane.
KWA SUALA LA JERRY MURO, KATIBU MKUU TFF ANGEACHIA NGAZI TU
Reviewed by Unknown
on
4:24 PM
Rating:
No comments: