ENDELEENI KUWATETEA AMBAO WAMEIACHA YANGA IKIENDA ALGERIA LAKINI HAWATA UKWEPA USALITI
NA SALEH ALLY
YANGA
imefunga safari kwenda nchini Algeria kuwavaa USM Alger ya nchini humo
katika moja ya mechi ngumu kabisa za Kombe la Shirikisho.
Kikosi
cha Yanga kimeondoka kinatia huruma, kikiwa na upungufu wa wachezaji
kwa kuwa wachezaji wake baadhi wameamua kutokwenda kutokana na masuala
kadhaa.
Wachezaji
hao wameona wasiende Algeria kwa kuwa kila mmoja ana madai yake lakini
suala lao limefanywa la kificho kwa kiasi fulani.
Ingawa
mambo yanakwenda kwa uficho lakini tunajua, Yanga ni klabu ya watu na
wenyewe ni Watanzania, hivyo hata kama jambo litafichwa vipi, mwisho
itajulikana tu.
Juhudi
za viongozi zimeonekana wanataka kutuliza mambo yaende kwa mwendo wa
kawaida kidogo, tumewaona wanajaribu kuwatetea wachezaji ili waonekane
hawajafanya jambo baya.
Inawezekana
wanaumia, lakini nao wanaona aibu kwa kushindwa kuwa watekelezaji
wazuri wanaoweza kufanya mambo vizuri na mwisho kuepusha hizo kero kama
ambazo zinazojitokeza.
Hivyo,
ili kuficha mambo na kutengeneza utulivu, basi ni juhudi za kuficha
mambo ili iwe salama kwa wote. Si jambo baya kwa kiongozi kutengeneza
busara na kufanya mambo kwenda kwa mwendo mzuri.
Pia
si vizuri kuficha ukweli kwa kuamini unayafanya mambo vizuri wakati
unaharibu kwa faida ya wachache huku ukijua si kutenda haki.
Taarifa
zilizopo, wachezaji hasa wale nyota au tegemeo waliogoma kuondoka ni
kwa sababu ya mishahara yao ya miezi kadhaa. Tumeelezwa ni miezi mitatu,
lakini hata kama itakuwa ni miezi miwili au mmoja, bado ni mishahara na
wanadai.
Kama
hawajalipwa kweli, basi wana haki, wanastahili kulipwa na kama
hawajalipwa basi hii si sahihi, walipwe. Maana wanafanya kazi yao
wanapambana na wanaumia, hivyo haki yao si jambo la kubembeleza.
Pamoja
na hivyo, bado ninarudi katika msimamo wangu uleule kwa kuwa katika
hili si jambo geni ninaloliandika kwamba kama umecheleweshewa mshahara,
hauwezi kususa kazi na kuacha chombo unachokiendesha, kiende mlama.
Binafsi
naona kufanya hivyo ni usaliti, naita usaliti kwa kuwa unakubali
unachokitumikia kitumbukie shimoni, hii ni kuonyesha hauna mapenzi ya
dhati na hasa kama unagoma katika kipindi cha uhitaji mkubwa.
Yanga
uliyoipigania iingie hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho. Leo
unagoma kwenda kuitumikia hata kama itafeli. Je, kama utalipwa mishahara
yako hapo baadaye, hii ya siku ambazo uliisaliti Yanga halafu ikaenda,
mfano ikafungwa, utailipa nini? Utachukua mshahara wa siku hizo?
Nakubaliana
na watu kudai haki zao, lakini bado kuna njia sahihi, angalau wachezaji
wangeenda kuipigania Yanga halafu wangerudi baada ya mapambano na
kuitisha mkutano wa waandishi wa habari na kuomba wasaidiwe na Wanayanga
na Watanzania kutokana na hali waliyonayo, mimi ningewaelewa.
Kuacha
Yanga izame, maana yake bado huna mapenzi. Hivyo kuna kila sababu ya
Yanga kuangalia upya tena watu walionao kama kweli wapo kwa nia ya
klabu. Kwa viongozi pia, basi waonyeshe hawajafeli kwa kuwa waendako,
chombo kitaenda mlama zaidi ya hapa na mwisho kuzama.
YONDANI:
Huyu
mkataba wake umeisha kwa zaidi ya mwezi na sasa, ajabu uongozi
umeshindwa hata kukaa naye mezani pamoja na umahiri wake. Ameamua kukaa
kando licha ya kuelezwa kwamba anaumwa.
TSHISHIMBI:
Kuna
taarifa za ndani zinaeleza kweli Mkongo huyu ameumia na hata mechi
dhidi ya Simba alicheza akiwa mgonjwa. Bado suala la mshahara
limechangia aumwe zaidi.
AJIBU:
Imeelezwa
hakuwa na ugonjwa wa kushindwa kwenda, kama ni maumivu aliyonayo na
mshahara wake ungekuwa umetoka, basi angejitutumua na kuungana na
wenzake Algeria.
CHIRWA:
Inajulikana
huyu si mara ya kwanza, aliwahi kususa na kwenda kwao Zambia, viongozi
wakamtetea lakini ikajulikana. Amerudia na huenda anaona ni jambo rahisi
na haoni shida, aliishaitoa Yanga Kombe la Mapinduzi na mshahara wake
akalipwa.
CANNAVARO:
Hongera
kwa kujitolea Yanga, lakini inaelezwa ana matatizo ya kifamilia. Kweli
sasa, kipindi ambacho Yanga inakwenda kuivaa timu ya Algeria, vipi
nahodha?
KAMUSOKO:
Tunaambiwa
ni majeruhi, lakini tunajua alishaanza kucheza na hakukuwa na taarifa
ya kuumia kwake. Hakuna ubishi, suala la utata wa mishahara, naye yumo
lakini kumbuka amekuwa nje zaidi ya hiyo miezi mitatu anayodai, na
amevumiliwa!
ENDELEENI KUWATETEA AMBAO WAMEIACHA YANGA IKIENDA ALGERIA LAKINI HAWATA UKWEPA USALITI
Reviewed by Unknown
on
3:44 PM
Rating:
No comments: